Kulingana na Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya ya mwaka 2015-2016, takriban theluthi ya watoto wote chini ya miaka mitano wana udumavu na asilimia 14 wana upungufu wa uzito. Sababu kuu zinazoongoza kuleta utapiamlo ni ukosefu wa lishe mchanganyiko na bora kwa kila kaya, upatikanaji mbovu wa huduma za afya (pamoja na maji safi na salama, usafi wa mazingira), na mienendo duni ya lishe. Hali ya upungufu wa damu kwa mama ni shida nyingine kubwa nchini Tanzania, ikiwa na asilimia 57 ya wanawake wajawazito na asilimia 46 ya mama wanaonyonyesha wanaathiriwa.
Kama sehemu ya mkakati kamili wa lishe, USAID inazingatia kupunguza kiwango cha udumavu nchini Tanzania kupitia mipango na huduma za afya na kilimo katika ngazi za wilaya na jamii. Uwekezaji muhimu kwenye lishe ni pamoja na: 1) Kuimarisha Taasisi za Serikali za Tanzania na asasi za kijamii (AZAKI) zinazoshughulikia masuala ya lishe; 2) Kuongeza juhudi za mabadiliko ya kijamii na mienendo ili kuboresha namna ya ulishaji wa watoto wachanga na wadogo; na 3) Kuongeza upatikanaji wa lishe yenye afya, lishe mbalimbali kwa mama na watoto. Mradi wa lishe wa USAID unaambatana kabisa na Mpango wa Utekelezaji wa Lishe ya Kitaifa wa Tanzania (2016-2021).