Tangu mwaka 2015, USAID imefadhili mradi wa upatikanaji wa chakula wa “Building Capacity for Resilient Food Security". Kwa miaka sita, USAID imekabidhi takriban Dola za Marekani milioni 5.3 kufadhili masuala ya hali ya hewa nchini Tanzania. Kupitia msaada wa kitaalamu kutoka FAO, mradi huu unasaidia TMA kuboresha usahihi wa taarifa za hali ya hewa kwa wakulima na watu wa mawasiliano, wanaojulikana kama "maafisa ugani." Kwa taarifa hizi zilizoboreshwa, wakulima wataweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu wakati wa kupanda na kuvuna mazao, na hivyo kuongeza uzalishaji na kipato.
Vifaa vya ufuatiliaji wa hali ya hewa na teknolojia ya hifadhidata ya huduma ya hali ya hewa vilivyokabidhiwa wiki iliyopita, inaruhusu TMA kukusanya takwimu za hali ya hewa ndani ya nchi.
"Vifaa vipya na seva ya hifadhidata vitaimarisha uwezo wa TMA kukusanya na kuhifadhi taarifa za hali ya hewa za ndani ya nchi. Hizi ni sehemu muhimu kwa usambazaji wa taarifa kwa wakati unaofaa na husaidia wakulima kutumia taarifa za hali ya hewa wakati wote wa kupanda na kuvuna, " alisema Mkurugenzi wa Ofisi ya Ukuaji wa Uchumi kutoka USAID, Terhi Majanen.
Vifaa na msaada wa teknolojia hii pia vitasaidia Tanzania kupanua uzalishaji na usalama wa chakula wakati wa mabadiliko ya hali ya hewa. Kupitia mpango kama huu, maendeleo endelevu yanawezeshwa na dhana ya kujitegemea inafikiwa.
“Kwa niaba ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Marekani na FAO kwa kushirikiana nasi, na kwa kufikia washirika wengine zaidi nchini Tanzania, na kutoa elimu juu ya utumiaji wa taarifa za hali ya hewa katika kilimo. Ufadhili wenu kwenye ununuzi wa vifaa maalumu vya kupima mvua na uboreshaji wa hifadhidata ya huduma za hali ya hewa ya kilimo ya wavuti ni muhimu sana kwa kuongeza upatikanaji wa takwimu na usahihi wa utabiri wa hali ya hewa, "Amesema Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi.
Ili kupata taarifa zaidi, tafadhali piga simu Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kupitia +255 22 229-4000 au barua pepe: DPO@state.gov.