Language

Zanzibar – Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright leo ametangaza msaada mpya kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar kusaidia jitihada za kubaini na kushughulikia milipuko ya maradhi, hususan janga la COVID-19.  Balozi Wright ametangaza msaada huo katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar (Zanzibar Public Health Emergency Operations Center – ZPHEOC), kilichoanzishwa kwa msaada kutoka Kituo cha Udhibiti wa Maradhi cha Marekani (CDC), Shirika la Afya Duniani (WHO) na taasisi ya Global Fund.  Balozi Wright alifungua kituo hicho katika hafla iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Afya wa Zanzibar Nassor Mazrui, Mwakilishi wa WHO, Dk. Ghirmay Andemichael na Mwakilishi wa Global Fund Nelson Msuya.

Lengo kuu la Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar (ZPHEOC) ni kubaini na kushughulikia kikamilifu na kwa ufanisi vitisho kwa afya ya umma.

Kituo hiki kipya kilichopanuliwa zaidi kitaongeza uwezo wa wataalamu wa afya ya jamii kudhibiti milipuko ya maradhi na kushughulikia dharura za kiafya kwa uratibu ulio mzuri zaidi na kwa ufanisi.

“Sisi sote ni sehemu ya dunia iliyoungana, hivyo sote tupo katika hatari ya maradhi yanayosambaa ndani na hata nje ya mipaka yetu. Madhara makubwa ya janga la COVID-19 katika mwaka uliopita, yametudhihirishia wazi jambo hili. Aidha, yametudhihirishia umuhimu wa kuwa na nguvu kazi iliyoelimishwa vizuri na kuwa na vyombo na mifumo yenye ufanisi inayoweza kutambua kwa haraka hatari zozote zinazojitokeza na kuchukua hatua za haraka kuzikabili,” alisema  Balozi Wright katika hotuba yake ya ufunguzi akielezea umuhimu wa ZPHEOC katika kudhibiti milipuko ya maradhi.

ZPHEOC kilianza mwaka 2019 kama taasisi iliyokuwa na chumba kimoja tu cha ofisi. Jengo la kituo kipya lilitolewa na Serikali ya Zanzibar na kukarabatiwa kwa msaada wa Global Fund na Shirika ya Afya Duniani (WHO). Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Marekani (CDC) kilitoa mafunzo kwa wataalamu wa epidemiolojia (ikiwa ni pamoja na watumishi wa Wizara ya Afya Zanzibar), kilisaidia kuanzishwa mfumo wa kufuatilia na kushughulikia matukio (incident management system) na kununua vifaa muhimu (vikiwemo vifaa vya mikutano ya video, projekta, gharama za kuunganishwa na mtandao wa internet na kulipia leseni ya programu za kompyuta inayotumika katika uendeshaji wa shughuli za kituo (EOC software licensing). Aidha CDC ilisaidia kutoa mafunzo kwa watendaji muhimu wa ZPHEOC kupitia programu yake ya ufadhili wa mafunzo ya namna ya kushughulikia dharura za afya ya jamii iitwayo Public Health Emergency Management fellowship program. Mafunzo hayo yalifanyika jijini Atlanta, Marekani.

Mbali na kusaidia jitihada za Wizara ya Afya ya Zanzibar za kudhibiti milipuko ya maradhi kupitia ufuatiliaji wa karibu (surveillance), kubaini na kuchukua hatua za kuzuia kuenea kwa maambukizi, serikali ya Marekani inachangia pia kwa kutoa fungu jipya la kusaidia utoaji matibabu muhimu kwa wagonjwa, ikiwemo wale walioathiriwa na janga la COVID 19, alitangaza Balozi Wright. Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na CDC wametenga zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 1.2 kusaidia jitihada za Wizara ya Afya za kukabiliano na milipuko ya maradhi. Fedha hizi ni sehemu ya uwekezaji muhimu katika usalama wa afya unaofanywa na Serikali ya Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Mwezi Aprili 2021, Serikali ya Marekani kupitia USAID ilitoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 400,000 kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar. Katika hafla hii ya uzinduzi, Balozi Wright alisema kuwa kiasi kingine cha ziada cha Dola za Kimarekani 500,000 kinatolewa na USAID ili kupanua huduma ya utoaji oksijeni na zile zinazohitaji uangalizi maalumu.

Msaada huu ambao utaelekezwa katika visiwa vyote vya Zanzibar, Pemba na Unguja utaboresha na kuongeza matumizi ya oksijeni, huduma za dharura na zile za wagonjwa mahututi. Mpango huu utalenga katika 1) kuinua uwezo wa wahudumu wa afya wanaotoa huduma za dharura na zile za wagonjwa mahututi, 2) kuimarisha uwezo wa mafundi sanifu wa vifaa tiba (biomedical technicians) kutumia, kutunza na kufanyia matengenezo vifaa vya oksijeni, na 3) kuongeza upatikanaji wa vifaa vya oksijeni katika hospitali na vituo vya afya vipatavyo sita visiwani Zanzibar.

Fedha kutoka CDC zitatumika kuimarisha shughuli za ufuatiliaji wa karibu wa maradhi na wagonjwa (surveillance) na uendeshaji wa shughuli za ZPHEOC.

“Kama inavyodhihirishwa na michango hii, hakuna shaka yoyote kwamba Marekani ipo bega kwa bega na Wizara, wahudumu wa afya na watu wa Zanzibar katika kupambana na COVID-19,” alisema Balozi Wright katika hotuba yake.

Image
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright ametangaza msaada mpya kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar kusaidia jitihada za kubaini na kushughulikia milipuko ya maradhi, hususan janga la COVID-19.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright ametangaza msaada mpya kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar kusaidia jitihada za kubaini na kushughulikia milipuko ya maradhi, hususan janga la COVID-19.
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzani