Dar es Salaam, Tanzania - Mwaka jana, UVIKO-19 ilisababisha janga la kidunia ambalo halikutegemewa kutokea. Hata hivyo malaria imekuwa tatizo kwa muda mrefu nchini Tanzania. Marekani inajivunia kuisaidia Tanzania kuendelea na mapambano yake dhidi ya malaria. Jitihada ambazo Tanzania imechukua kuendeleza huduma muhimu za malaria zinaokoa maisha ya watu wengi.
Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI) umeshirikiana na Tanzania kupambana na malaria tangu 2006, na kuchangia dola za Marekani milioni 176 katika miaka minne iliyopita. Ufadhili huu umewasilisha vyandarua vyenye viatilifu, dawa za kuokoa maisha, upimaji wa kiwango cha juu na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya zaidi ya 4,700 hadi sasa. Kupitia ushirikiano wa karibu na watu, taasisi na serikali ya Tanzania, serikali ya Marekani pia inaimarisha mifumo ya afya kuimarisha na kuongeza juhudi za Tanzania kumaliza ugonjwa huu hatari, lakini unaoweza kuzuilika kabisa. Maendeleo makubwa ya Tanzania dhidi ya malaria yameangaziwa katika Ripoti ya 15 ya Mwaka ya Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria. Kwa mfano, umiliki wa vyandarua vyenye viatilifu umeongezeka hadi asilimia 78 (kutoka asilimia 23 mwaka 2005). Kulala kwenye vyandarua vyenye viatilifu huzuia mbu wakati wa usiku, wakati wana nafasi kubwa ya kuuma, na kuua mbu wanaotua kwenye chandarua. Hivyo, kupunguza kuenea kwa malaria.
Wakati wa mahojiano ya hivi karibuni na kituo cha Clouds FM kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani, Mkurugenzi Mkazi wa USAID Andrew Karas alisema, "Uwekezaji wa PMI unasaidia na kujenga juu ya yale mambo muhimu yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania. Ufadhili wetu unalingana na vipaumbele vya Tanzania vilivyoainishwa katika Dira yake 2025 yenye kuzingatia kuendeleza watendaji wa kazi, na pia taasisi na mifumo ambayo serikali inaona ni muhimu kufikia na kudumisha dira yake ya muda mrefu. "
Licha ya maendeleo mazuri, watu wengi bado wanakosa hafua dhidi ya malaria tunazojua zinaokoa maisha. Lazima tufikie ambao hawajafikiwa. Wauguzi wengi, wakunga, wahudumu wa afya ya jamii na wengine wanatoa huduma muhimu za malaria bila mafunzo ya kutosha, vifaa, na malipo. Lazima tuifanye mifumo ya afya kuwa salama zaidi na bora kwa watu wanaowahudumia. Hatua muhimu ya kutokomeza malaria bado zipo mbali sana kwa nchi nyingi. Lazima tujitahidi kutokomeza malaria haraka.
Mratibu wa Malaria Ulimwenguni wa Marekani Raj Panjabi, aliyeteuliwa na Rais Joe Biden kuongoza Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI), anasema, "Sayansi inaonesha tunaweza kuishinda malaria na tunaweza kuitokomeza kipindi chetu. Walakini tunahitaji hatua ya ujasiri kuzuia UVIKO-19 isiturudishe nyuma. Marekani inajivunia kushirikiana na Tanzania kuendeleza mapambano. ”
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani kupitia DPO@state.gov.